Waziri Mkuu Mizengo Pinda amezindua rasmi mradi wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wajasiriliamali wadogo wanawake nchini uitwao MWEI na kuwataka wautumie kwa kujiletea maendeleo ikiwemo kuunga vikundi vya ushirika vya kuweka na kukopa.
Mradi huo umeanzishwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania kupitia kitengo chake cha kusaidia jamii(Vodacom Foundation) ili kuimarisha azma ya kusaidia jamii mbalimbali nchini ikiwa kama mshirika wa maendeleo pamoja na ustawi wa wananchi kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo na hata zile zinazobuniwa na taasisi hiyo.
Akizindua mradi huo katika kijiji cha Bwigiri mkoani Dodoma Waziri Mkuu Pinda amesema kupitia mradi huo Vodacom itawapa wajasiriamali wadogo wanawake mikopo isiyo na riba hivyo watumie nafasi hiyo kurudisha kwa wakati huku ili mradi huo uwafikie na wengine.
“Kumekuwa na kawaida kwa wanawake kutumia fedha za mikopo kwa kununua kanga na kuwapa wanaume zao fedha za pombe. Nyie nawaomba msifanye hivyo, kopeni, ibueni miradi, rudisheni MWEI kwa wakati na muanzishe kikundi chenu cha kuweka na kukopa kwa riba ili mjipanue zaidi,” alisema Pinda.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Tanzania Mwamvita Makamba ametaja malengo ya MWEI na kusema hadi kufikia mwaka huu tayari mradi huo umeshatoa mikopo kwa akina mama 4500 mikopo yenye thamani ya shilingi Milioni 90 na mkakati ukiwa kuwafikia wanawake 10,000/- kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Akifafanua Makamba amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo hutumia mfumo wa Huduma ya Vodacom M Pesa na muombaji hupokea mkopo na kurejesha kwa njia hiyo. Wakala wa huduma hiyo wameenea nchi nzima hivyo kumwezesha muombaji kutumia gharama nafuu zaidi na kwa urahisi kufikia huduma hiyo na kupata fedha.
“Tunatambua kuwa changamoto kubwa katika eneo la uombaji mikopo sit u kupitia mradi huu wa MWEI bali mahali popote pale ni namna ya kupangilia vema matumizi ya mkopo na utunzaji wa kumbukumbu za mkopo kwa mwombaji,” Amesema Mwamvita.
Kabla ya wapewaji mikopo kuwezeshwa wanapatiwa mafunzo na Shirika la Viwanda vidogo SIDO kwa gharama za Vodacom Tanzania kupitia mfuko wa Vodacom Foundation ambao ndio waratibu wa mradi wa MWEI.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wajasiriamali wadogo wanawake wa kijiji cha Bwigiri Claudia Goda alisema kwa kuwa kampuni hiyo imeonesha nia ya kuwasaidia watahakikisha wanaendeleza mitaji waliyopewa na hatimaye wajikwamue kutoka katika umasikini.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwaonesha baadhi ya wajasiriamali wadogo wanawake nembo ya mradi unaowawezesha na Kuwajengea Uwezo wajasiriamali wadogo wanawake MWEI ulioanzishwa na Vodacom Tanzania ili kuwapa mikopo isiyo na riba mara baada ya kuuzindua mwishoni mwa wiki kwenye kijiji cha Bwigiri mkoani Dodoma.Wanaoshudia (Katikati) Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Dietlof Mare na Afisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa kampuni hiyo Mwamvita Makamba.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda (Kulia) akiteta jambo na Afisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Tanzania Bi Mwamvita Makamba kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa Kuwapa mikopo isiyo na riba kwa wajasiriamali wadogo wanawake MWEI utakaowezeshwa na huduma ya M Pesa inayotolewa na Vodacom uliofanyika mwishoni mwa wiki kijiji cha Bwigiri mkoani Dodoma. Mpaka kufikia Julai 2011 tayari wanawake 4500 wamefikiwa na kukopeshwa shilingi milioni 90/-.
KULE KWETU UCHAGANI TUNAITWA SUMANAAA.....izo shanga maza alizotinga hapo juu kwenu je?